Home Ads


Halmashauri ya Babati yaingia Mkataba na J.P TRADERS.


Wananchi wa tarafa za Mbugwe na Gorowa wilaya ya Babati mkoa wa Manyara wanatarajiwa kuwa na miundo mbinu mizuri ya barabara baada ya mkandarasi kupatikana na kusaini mkataba tayari kwa kuanza ukarabati wa bara bara hizo.
 Meneja wa kampuni ya J.P TRADERS COMPANY LTD iliyoingia makataba na Halmashauri ya wilaya ya Babati Gabo Mathias Makelegwa alisema katika zoezi hilo la utengenezaji  wa bara bara,ajira 50 zitazalishwa ambapo wakazi wa maeneo husika watanufaika kwa kupata ajira hizo  na kukuza mawasiliano ya kiuchumi baina ya tarafa hizo na mkoa.

Makubaliano ya utengenezaji wa barabara hizo umetiwa saini jana baina ya Halmashauri ya wilaya ya Babati na kampuni ya J.P.Traders Ltd ya Dar es salaam ambapo utengenezaji wa barabara za tarafa ya Mbugwe utaragharimu jumla ya shilingi milioni 113,323,920.

Mhandisi wa ujenzi wa barabara wa Halmashauri ya wilaya ya Babati, Innocent Mlay alizitaja barabara za tarafa ya Mbugwe  kuwa ni kutoka Vibao Vitatu hadi Kiru Six, Magugu-Mapea na Kisangaji, Magara-Mayoka hadi Maji moto na Minjingu hadi Kakoi.

Alizitaja barabara kutoka Tarafa ya Gorowa kuwa  ni kutoka Endaberg, Riroda hadi Managhat, Boay, Gidas hadi Bubu, Riroda, Duru hadi Bubu na barabara ya kutoka Endanachan hadi Gidas zitakazogharimu shilingi Milioni 103,444,000.

Mhandisi Mlay alifafanua kuwa kazi ya ujenzi wa barabara hizo unatarajiwa kuanza wiki mbili baada ya kusainiwa kwa mkataba na kwamba zinatarajiwa kukamilika kwa miezi minne kwa kuwa kazi zitakazofanyika ni za  kutengeneza Makalvat, Mitaro na kuweka Vivuko katika baadhi ya maeneo ya barabara hizo.
Kwa maana hiyo mkandarasi ataanza kazi rasmi mwanzoni mwa mwezi august 2016.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Babati,Nicodemus Tarmo alimtaka mkandarasi huyo kufanyakazi kwa uaminifu na uadilifu na kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa kwa kuwa muda wa wiki mbili  toka kutiliana saini utaisaidia kampuni  hiyo kufanya maandalizi ya vitendea kazi na wafanyakazi.

“Baada ya ushindani mkubwa wa kumpata mkandarasi aliyekidhi vigezo, tunaimani kampuni hii itakamilisha kazi kwa wakati uliopangwa na kufanya kazi kwa kuzingatia ubora. Alisema Tarmo.

Makubaliano hayo yalifanyika mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Babati, Hamisi Malinga aliyeanza kazi rasmi baada ya kuteuliwa kwake na kukabidhiwa ofisi hiyo Jumatatu tarehe 18 july 2016.

No comments:

Powered by Blogger.