Home Ads


Arumeru wamuunga mkono Magufuli kuzuia mikutano.


BARAZA Kuu la Waislamu (Bakwata) wilayani ya Arumeru mkoani Arusha, limeunga mkono kauli ya Rais John Magufuli ya kusitisha mikutano ya hadhara ya kisiasa na kutaka watu kufanya kazi ili kuinua uchumi wa nchi.
Bakwata imesema kauli hiyo inapaswa kuungwa mkono na wananchi wote nchini na kuongeza kuwa siasa zisizokwisha, zinaweza kuyumbisha Watanzania na kuwafanya waache kufanya kazi na kuanza kuzungumza siasa katika muda wa kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Arumeru, Mwenyekiti wa Bakwata wilayani humo, Shehe Haruna Hussein, alisema kila kitu kina muda wake na mwisho wake, hivyo siasa zilikuwa na muda wake na sasa muda huo umekwisha, kinachofuata ni kufanya kazi kwa lengo la kujenga nchi na sio vinginevyo.
Alisema wao kama Bakwata wilaya ya Arumeru wanaunga mkono kauli ya kiongozi huyo ya kusitisha shughuli zote za kisiasa ikiwemo mikutano ya kisiasa na kutoa rai kwa wana siasa kutumia fursa hiyo kufanya kazi ya kuinua uchumi wa taifa Shehe Hussein alisema kauli ya Rais Magufuli inaweza kutafsiriwa tofauti, lakini ikiichunguza sana ina maana kubwa sana hivyo Bakwata inaunga mkono kwa sababu imeona mbali na kuamua kuiunga mkono kwa asilimia mia moja.
Akizungumzia utendaji kazi, Bakwata imemshauri Rais Magufuli kuwatumia baadhi ya viongozi wenye uzoefu na rekodi nzuri ya utendaji katika awamu zilizopita ili waweze kumsaidia kuboresha utendaji kazi katika serikali yake ya awamu ya tano.
Alisema Bakwata inaunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli katika kujenga serikali yake ila inatoa rai kwa Rais huyo kutowasahau wazee wenye busara na utendaji wao mzuri wa kazi.
Aidha baraza hilo lilimtaja aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani na naibu waziri mkuu Dk Augustine Mrema kuwa ni moja wa viongozi wenye historia kubwa na utendaji kazi hasa falsafa yake aliyokuwa akitumia ya kutoa siku 7 katika kuwabana na kuwajibisha watendaji wabovu ambapo kwa kiasi kikubwa ilifanikisha kuwanyoosha watendaji hao.
Aidha walimtaka Rais Magufuli kuendelea kuwabana watendaji wabovu ambao hawataki kuendana na kasi yake katika kutekeleza majukumu ya kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto za maisha zinazowakabili.
Alisema Bakwata itaendelea kuliombea taifa pamoja na Rais Magufuli hili kila hatua anayoifanya iwe na Baraka zake mungu na kuomba mwenyezi mungu kumtangulia popote anapo kabiliana na kutokomeza ufisadi, rushwa wizi pamoja na wahujumu uchumi na wenye nia ovu na serikali yake.

No comments:

Powered by Blogger.